“Waonekana mahiri wa lugha na mwenye busara katika kujibu maswali. Majina yako kamili waitwa nani?”, akaniuliza. Mara hii niliweza kuona tabasabu usoni mwake. “Kwa majina naitwa Kazamoyo Juma”, nikamjibu. Uso wake uling’aa mara moja. Sikujua ni kwa nini. Kwani alifahamu jina langu? Nikawaza. “Kazamoyo…kaza…Moyo. Unatoka wapi?”, akaniuliza bwana yule. “Nimetoka kaunti ya Hesabika mjini Weusisi”, nikamjibu. Bwana yule aliruka kutoka kwenye kiti chake na kunikumbatia. Machozi yalimdondoka. Alikuwa amenifahamu. Alikuwa binamu yangu Taru. Katika harakati hiyo niliweza kujiwa na fahamu zangu na kujua kuwa wakati wangu ulikuwa umewadia. Kumbe kutoka siku ile aliponipa kazi katika kampuni yake alikuwa hajanifahamu? Sadfa ilikuwa imetukutanisha.