“Nikumbukapo mashaka tipitipi yaliyoizonga familia yetu naamini kuwa ulimwengu umefurika malimwengu ya kila nui ambayo hukingama mbele ya walimwengu maishani na kusababisha pandashuka. Kama barabara ndefu ilivyo safari ya Maisha haikosi mabonde, vilima, milima, tambarare na kona. Je. Ni gurufu gani isiyokuwa na gurufu? Kwa bahati njema mawimbi ya safari ngumu hayadumu maishani, huisha namna Maisha yenyewe yanavyoisha.
Baadhi ya Pandashuka ni furaha na huzuni, raha karaha, vicheko na vilio, utajiri na umaskini, shibe na njaa, amani na vita, afya njema na maradhi, upendo na chuki n ahata shwari na shari namna wasemavyo wengine. Kimsingi, pandashuka hutusambazia ama utulivu au uchungu nzima unaozaa jakomoyo sufufu. Je, ni nani asiyejua kuwa painamapo ndipo painukapo?”
"Ni riwaya ya kitawasifu inayomfahamisha msomaji kutalii katika usimulizi aula uliosukwa kwamba ni mlo wa kisanaa kwa kukolezwa mbinu kemkem za sanaa. Mwandishi aliyetopia na kugharika ukwasi wa lugha ameyatumia maneno ya kawaida namna isiyo ya kawaida ili kuukamilisha ubunifu usio na kifani. Mwandishi huyu mahiri amesimulia visa tele vinavyoingiliana na kuunda taswira halisi za pandashuka katika jamii..." Tahakiki ya Fatma Ali Mohamed(Zanzibar)