Fasihi simulizi ya Kiafrika ni tamu sana. Utamu wake unaanzia katika ukweli kwamba si kazi ya sanaa ambayo hulenga kumburudisha tu Mwafrika au msomaji, bali ni sanaa ya lugha ambayo ni sehemu ya maisha ya Mwafrika mwenyewe. Kila ilipo jamii ya Kiafrika, kuna fasihi yake. Kitabu hiki, ambacho kimeandikwa kwa umakini, si kwamba kinatukumbusha fasihi yetu ya zamani, bali kinaturai kwamba fasihi simulizi tunaiishi kila siku. Fauka ya hayo, kazi hii inatuzamisha katika maarifa adhimu yanayotuhusu wenyewe na ulimwengu wetu unaobadilika kila kukicha.
Kitabu hiki cha Bw. Kitsao, kimeandikwa kwa ufundi wa hali ya juu na uliotukuka. Nilipousoma mswada wake, nilitamani niurudie mara kadhaa kutokana na utamu wake. Kwa hakika, chapisho hili ni bahari ya maarifa yetu ya Kiafrika. Mimi nimeogelea nikachota yangu. Ninakukaribisha nawe msomaji, ujitose ndani ili upate raha na maarifa niliyopata. Hongera sana Mwl. Kitsao kwa kutuandikia kazi nzuri sana.
(Leonard Bakize, Mhadhiri wa Kiswahili - Chuo Kikuu cha Zimbabwe)